WEWE NI KAMA NGURUWE NA KAMA NANASI |BY PRINCE BEWISA - Fahamu zaidi Staili za Maisha na Saikolojia. Bewisa App | ™ - Efe. 5:15-17
SOMA HIZI PIA:
Loading...

WEWE NI KAMA NGURUWE NA KAMA NANASI



UNAWEZA KUPATA STORI ZETU MOJA KWA MOJA KWA KUBONYEZA 'LIKE' HAPA



« Piga 0652262137 kuweka tangazo lako hapa - Push kwa Buku tu »

 

Nguruwe ni mnyama ambaye tabia yake kwa maana ya haiba ya usafi (hygiene) si nzuri sana ingawa watu wanaojihusisha na hoja za kisaikolojia (facts) husema kuwa nguruwe ni mnyama msafi.

Kwa sisi ambao tumewahi kuishi na hawa wanyama tuna ukweli fulani juu ya maisha yao. Ni wanyama wasafi ama wachafu kulingana na mazingira waliyopo na usimamizi. Ila kitabia, unaweza kumwogesha lakini asijali kuwa umemwogesha akarudi tena kwenye matope kama kawaida. Na ndio maana Biblia inadharau kumfunga nguruwe pete ya dhahabu puani (Mith. 11:22)

Licha ya namna ambayo unaweza kumwona nguruwe kwamba kuna wakati anaweza kuwa mchafu, mharibifu (maana pia ni mharibifu mzuri sana usipomfungia), na asiyekuwa na haiba ya usafi kiakili lakini huyu mnyama amefanya watu kutofautiana kiimani kwa sababu tu ya utamu wa nyama yake.

Nyama ya kitimoto (kama nakuona vile mate yanavyokutoka) ni tamu sana na binafsi huitumia (naongea kama msimulizi). Wengi huiita majina kulingana na mahaba yao kwa nyama hiyo, imani na pia tafsida ili kutokuwakera wale wasioitumia na pengine haramu kwao. Huiita kitimoto, noah, mdudu, n.k na ni nyama yenye thamani sana buchani zaidi ya pengine mbuzi, samaki, kuku na ngombe hapa Dar es Salaam ingawa kwa mikoa mingine yaweza kuwa tofauti. Hapa Dar es Salaam bei yake kwa kilo ni kati ya 10,000 mpaka 15,000 rosti ama mbichi kwa bei za rejareja.

Tuachane na kitimoto na turudi kwa kiumbe kingine ambacho ni mmea na tunda tamu sana. Hapa namaanisha NANASI. Tunda hili linapatikana karibia asilimia 70 – 90 ya mikoa yote hapa Tanzania ingawa wingi wake unatofautiana kati ya mkoa na mkoa, mahali na mahali. Kwa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam nanasi linapatikana sana na hasa kipindi cha msimu wake basi kila nyumba lazima ipate nanasi walau mara moja kwa wiki kwa wastani wa chini sana maana bei ya nanasi huweza kufika mpaka 500 kwa nanasi dogo na kutokuzidi 3,000 kwa nanasi kubwa msimu wa mananasi (high season).

Nanasi ni tunda ambalo kwa nje lina majani na miiba ambayo hulifanya lisikutamanishe sana likiwa shambani na kwa waoga wa kuchomwa na vijimiiba vyake huenda wasiweze kulivuna shambani (ahahahaha….). na si ajabu pia hata likivunwa kuna ambaye pia hawezi kuliandaa kwa maana ya kulimenya kutokana na miiba yake na aina ya ganda lake kwa nje. Kifupi unaweza kujiuliza kwa namna lilivyo hivi ni nani aligundua kuwa ni tunda linalofaa kuliwa?

Licha ya changamoto za nanasi kwa namna lilivyo, kwakweli ni tunda tamu sana na sidhani kama kuna mtu ataniambia “mwalimu mimi sipendi kabisa nanasi”. Kwanza harufu yake hushawishi na pia ladha yake hukuna mpaka kisogoni. Ni kama naona unavyolitamani, eti e?

Sasa ngoja nitoke kwenye kusimulia halafu nifundishe kitu hapa na kukutia moyo mtu wa Mungu. Kwanza kwanini nianze kwa simulizi za Nguruwe na Nanasi?

Inawezekana wewe ni Nguruwe kabisa au Nanasi kabisa. Usinune ukasema mtumishi amekutukana, la hasha. Maisha yako kwa watu yanaweza yakaonekana kama nguruwe kabisa na mimi nakubaliana na hao watu kabisa kwamba wewe ni kama nguruwe.

Lakini pia wewe ni kama nanasi kabisa kulingana na changamoto ulizonazo na hali unayopitia. Ukijiangalia unasemwa vibaya, watu hawajui zuri lako ulilowatendea hata moja na wengine wanakutukana kwa msaada na wema wako kwao, pengine una madeni makubwa yasiyolipika kirahisi na kwa wakati na umeishi katika wakati mgumu sana na huna namna ya kufanya, ndugu wamekutenga, biashara imejaa hasara na huoni faida yake kiasi kwamba unatamani uiache, kazini ni vimbwenga kila siku na kuna wale kina nanii mara zote wamekuwa zaidi ya vijipu uchungu kwako hata huna amani na kazi yako, na mambo mengine kibao ambayo yanatupa dhiki za kidunia; hayo tunayaita miiba na wewe katikati ya miiba ni nanasi. Usikate tamaa, mngoje Bwana bado wewe ni “mtamu” mfano wa nanasi. Bila miiba bado wewe si mtamu, hiyo miiba ipo ili kuboresha ladha yako tamu.

Aibu, tabia mbaya, dhambi, uovu, mateso, kudharauliwa, n.k huo ni uchafu mbele ya nguruwe na huenda unaogelea humo na watu wameshakuhukumu hufai lakini nia ya kuwa msafi unayo na ndio maana kila wakiitwa watu kutubu unaenda, wakiitwa wanotaka kuokoka basi na wewe umo, Neno likihubiriwa basi unakazana kulisikia na unaomba, lakini kuna dhambi inakuzonga kwa upesi, kuna aibu ipo malangoni mwako, kila ukijitahidi kutoka unashindwa na watu wameshakuhumu; wewe ni kama nguruwe. Ni nje tu u mchafu lakini ukichinjwa wewe ni mtamu sana. Namaanisha una kitu cha thamani sana ndani yako, kazana kuomba mkono wa Mungu ukuvushe hapo na ufute aibu yako kama alivyofanya kwa mji wa Gilgali (Yosh. 5:9), unafaa sana usisikilize maneno ya watu wala hukumu zao, jitambue kuwa umependwa na Bwana na kwamba Yeye hawazi kama watu wala hasikilizi humu zao ili akutendee wewe wema wake bali analitazama Neno lake na Ahadi yake maishani mwako ili atimize.

Yesu alimwambia Herode neno hili baada ya Herode kumzonga kwa maswali mengi na makwazo, “Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.” – Lk. 13:32

Alimuita “mbweha” kwa sababu mbweha hubweka hovyo bila sababu na wala asijue kwanini anabweka na kwa wakati gani na wala lengo la kubweka hajui. Na mimi nikuambie ukweli kuwa hao wanaosema hovyo na kukunyanyasa na kukufanyia ubaya wasamehe bure tu maana hawaujui ukweli wa maisha yako. Ni kama mbweha tu. Na hakika ukikaa nyumbani mwa Bwana sawasawa na kuling’ang’ania pindo la vazi lake hutakosa kusamehewa na “siku ya tatu” utauona uweza wake kwenye maisha yako na hapo ndo utakuwa kama kitimoto mezani, mtamu na unavutia kwao, ni kama nanasi, mtamu na unavutia kwao. Ndipo na wewe utauimba wimbo mpya wa Bwana maishani mwako kama Hanna; Usikate tamaa, hilo tu!

Nimalize kwa kukuambia kuwa, hapo ulipo ni daraja la kesho yako, kuwa makini sana na uvumilie na kusamehe mabaya. Usitafakari mambo ya jana wala kuwabeba watu moyoni mwako. Wewe ni wa thamni na kesho yako ni bora mno kuliko jana na hata kuliko leo. Biblia inasema hivi;

“Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.” – Isaya 40:28-31

Mungu akubariki sana mtoto wa Mungu.

Naitwa Benson Mmari

Ili kupata Makala zaidi na kwa njia rahisi, Install App yetu kwenye PlayStore. Tafuta BEWIS APA, au BONYEZA HAPA



TUAMBIE UNA MAONI GANI JUU YA HILI?

Facebook Plugin by princebewisa

Chapisha Maoni

Enenda kwa hekima, ukijua ni yapi yaliyo mapenzi ya Mungu huku ukiukomboa wakati. Install Bewisa App kwenye PlayStore kwa maarifa zaidi.
- EV. BENSON W. MMARI, +255 768 111 279

CodeNirvana
© Copyright Bewisa App | ™ - Efe. 5:15-17 | Modified By PB Web and Graphics
Back To Top