NAMNA MKRISTO ANAVYOANGUKA KWENYE ZINAA |BY PRINCE BEWISA - Fahamu zaidi Staili za Maisha na Saikolojia. Bewisa App | ™ - Efe. 5:15-17
SOMA HIZI PIA:
Loading...

NAMNA MKRISTO ANAVYOANGUKA KWENYE ZINAA



UNAWEZA KUPATA STORI ZETU MOJA KWA MOJA KWA KUBONYEZA 'LIKE' HAPA



« Piga 0652262137 kuweka tangazo lako hapa - Push kwa Buku tu »

Na Mwl. Christopher Mwakasege


   Kila mara nilipopata habari za watu wa Mungu walioanguka katika dhambi ya zinaa nilikuwa najikuta najiuliza swali hili, “Hivi wanapataje ujasiri wa kutenda tendo hilo?”

          Akili yangu ilikuwa inakataa kabisa kuamini kuwa mtu aliyeokoka (na wakati mwingine amejazwa Roho Mtakatifu) anaweza kuanguka kwenye dhambi ya zinaa. Lakini hata hivyo bado nikawa naendelea kusikia majina ninayoyafahamu ya watu wa Mungu waliookoka waliokubwa na dhambi ya zinaa.

“Wanafanyaje mpaka wanaanguka katika zinaa”? Hili swali lilinisumbua kwa muda mrefu. Na siku moja nilikuwa nyumbani kwangu nikijiuliza swali hili moyoni, nikasikia Roho Mtakatifu akiniuliza ndani ya moyo wangu, akisema, “ Kwani Daudi aliangukaje? Je! Umesahau ya kuwa naye alikuwa mtu wangu, mtumishi wangu niliyempaka mafuta?

          Niliposikia swali hili, nilichukua biblia na kusoma maneno yanayoeleza kuanguka kwa Mfalme Daudi katika dhambi ya zinaa na mke wa mmoja wa askari wake.

          Mambo niliyoyasoma yalinifungua macho kuona jinsi ambavyo hata hivi leo watu wa Mungu wanavyoanguka au wanavyoweza kuanguka katika dhambi ya zinaa.

          Chukua biblia yako na usome habari hizi katika 2 Samweli 11:1-27 na 2 Samweli 12:1-25.

          Chanzo cha kuanguka kwa Mfalme Daudi katika dhambi ya Zinaa, ni KUTOKWENDA VITANI PAMOJA NA ASKARI WAKE.

“Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote, wakaangamiza wana wa Amoni, wakakuhusuru Raba. LAKINI DAUDI MWENYEWE AKAKAA YERUSALEMU”. (2 Samweli 11:1)

          Kama kiongozi wao, Daudi alitakiwa kuongozana na watu wake vitani, lakini yeye aliamua kubaki Yerusalemu asiende vitani, na akamtuma mtu mwingine amwakilishe. Na jambo hili lilimpa nafasi nzuri sana ibilisi ya kumpa Daudi kazi nyingine ya kufanya. Ni kazi gani hiyo?

“Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, AKATEMBEA JUU YA DARI ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke ANAOGA; naye huyo mwanamke alikuwa MZURI SANA WA KUPENDEZA MACHO”. (2 Samweli 11:2)

Ni kitu gani kilimfanya Mfalme Daudi aamue kutembea juu ya dari ya jumba lake badala ya kwenda vitani pamoja na watu wake? Na alipomwaona Bathsbeba, mkewe Uria akioga alishindwa kujizuia, mwisho wake ni kuzini naye na huyo mama kupata mimba!

Wakristo wengi wamejikuta wameingia katika mtego wa zinaa kwa sababu ya kutokwenda ‘Vitani’ wakati wanapotakiwa kufanya hivyo. Vita tunavyovisema, si vita vya kimwili.

“Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili, maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome; tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo”. (2 Wakorintho 10:3,4)

Na pia imeandikwa; “ Kwa maana kushindani kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili juu ya majeshi ya pepo wabaya, katika ulimwengu wa roho”. (Waefeso 6:11)

Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “ Kesheni mwombe msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” (Mathayo 26:41)

Usipovipiga vita katika maombi, inakuwa ni rahisi sana kuangushwa na majaribu unapokutana nayo. Wakristo wakipoa katika maombi inakuwa rahisi kuanguka katika dhambi, si katika zinaa peke yake, bali katika mtego wowote ambao shetani anauweka mbele yao!
Kutokuwa mwombaji, ni sawa na kutokwenda vitani na wenzako, kama vile Mfalme Daudi alivyofanya.

Kwa hiyo unaona ya kuwa ingawa Mfalme Daudi alikuwa mtu wa Mungu, mtumishi wake, na mpakwa mafuta wake, alianguka katika zinaa. Na hata hivi leo kuna wakristo, tena wameokoka, na kupakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu, wanaonguka katika dhambi ya zinaa. Kwa nini? Kwa kuwa hawavipigi vita vya kiroho na wenzao, na wamepoa katika kumtumikia Bwana.

Je! Lutu aliangukaje?

Hili ni swali ambalo Roho Mtakatifu aliniuliza baada ya kunieleza habari za Mfalme Daudi. Ingawa Lutu alikuwa mtu wa Mungu, na licha ya kuwa alikuwa anabebwa kwa maombi ya Ndugu yake Ibrahimu, bado alianguka katika zinaa.

Roho Mtakatifu alikuwa anaendelea kunijibu swali nililokuwa najiuliza ya kuwa, watu waliookoka wanaangukaje katika zinaa?

Habari za kuanguka kwa Lutu zimeandikwa katika kitabu cha Mwanzo 19:30-38.

Lutu alizini na watoto wake wawili wa kike baada ya kuleweshwa mvinyo.
Na ukiisoma habari hii inasikitisha sana. Shetani alipata nafasi ya kumwangusha Lutu si kwa sababu ya binti zake kumlewesha mvinyo, bali kwa kuwa MKE WAKE HAKUWA PAMOJA NAYE. Unadhani mke wake angekuwapo hawa watoto wangepata nafasi ya kumlaghai baba yao? Hapana! Kwa nini?
Kwa maana “ Bwana ameumba jambo jipya duniani, mwanamke atamlinda mwanaume.” (Yeremia 31:22)

Unaweza kujiuliza ni kwa njia gani mke atalimnda mume wake. Kumbuka imeandikwa mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana. Kazi moja ya busara iliyo ndani ya mke ni kumlinda mume kutokana na mashambulizi ya Malaya! Soma Mithali 2:11-22.

Hata hivi leo ndoa ambazo mume na mke hawakai vizuri, huwa ni rahisi kwa wao kuanguka katika dhambi ya zinaa hata kama wameokoka. Na huu siyo ushuhuda mzuri.
Tunamshukuru Mungu kwa wale ambao wamesimama katika ushuhuda ingawa ndoa zao zina matatizo.

Jambo la kujifunza zaidi

Roho Mtakatifu alipokuwa anaendelea kunifundisha akasema ndani ya moyo wangu hivi; “Watu wengi wanadhani zinaa ni tendo la kimwili tu linalofanywa kati ya mwanaume na mwanamke nje ya ndoa, lakini kuna namna zaidi ya moja unayoweza kuanguka katika zinaa.”

Niliposikia hivyo moyoni mwangu, niliichukua Biblia na nikaanza kuisoma upya juu ya zinaa na nikaona kuna namna nne ambazo zinaa inatajwa:-

1.     KATIKA MWILI:
“….Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili. Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya Kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? …. Ikimbieni zinaa, kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” (1 Wakorintho 6:13-20)

2.     KUTAMANI KWA MACHO. Yesu Kristo alisema;
“Mmesikia kwamba imenenwa Usizini; lakini mimi nawaambia, kila mtu AMTAZAMAYE MWANAMKE KWA KUMTAMANI, amekwisha KUZINI NAYE MOYONI MWAKE.” (Mathayo 5:27,28)

3.     KUACHA MKE NA KUOA MWINGINE
Yesu Kristo alisema;
“Kila amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine azini ……” (Luka 16:18)

4.     KUOA ALIYEACHWA. Yesu Kristo alisema;
“Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; NAYE AMWOAYE YEYE ALIYEACHWA NA MUMEWE AZINI.” (Luka 16:18)

          Kila mtu na ajipime katika hayo; ikiwa umefanya mambo kama hayo niliyoyataja, biblia inasema UMEZINI! Je       Hakuna waliokoka wanaofanya mambo ya jinsi hii? Wanaowaacha wake zao halali? – Wanaooa walioachwa? – na wanaozini katika mwili?

Na Mwl. CHRISTOPHER MWAKASEGE

SOURCE: http://www.mwakasege.org

Ili kupata Makala zaidi na kwa njia rahisi, Install App yetu kwenye PlayStore. Tafuta BEWIS APA, au BONYEZA HAPA



TUAMBIE UNA MAONI GANI JUU YA HILI?

Facebook Plugin by princebewisa

Chapisha Maoni

Enenda kwa hekima, ukijua ni yapi yaliyo mapenzi ya Mungu huku ukiukomboa wakati. Install Bewisa App kwenye PlayStore kwa maarifa zaidi.
- EV. BENSON W. MMARI, +255 768 111 279

CodeNirvana
© Copyright Bewisa App | ™ - Efe. 5:15-17 | Modified By PB Web and Graphics
Back To Top