UNAWEZA KUPATA STORI ZETU MOJA KWA MOJA KWA KUBONYEZA 'LIKE' HAPA ➞
« Piga 0652262137 kuweka tangazo lako hapa - Push kwa Buku tu »
Na;
Mw. Benson Mmari
Miongoni
mwa mambo tata kwenye jamii ni suala hili, yaani nani anapaswa kupiga goti
wakati wa kuvisha pete ya uchumba? Kumekuwa na mjadala mkubwa sana juu ya jambo
hili na majibu ni mengi lakini kwa bahati mbaya wengi wanatoa majibu kulingana
na mapokeo ya wazungu au pia utamaduni wa kabila lake, utashi na hata namna
alivyolelewa hasa mfumo wa familia yake katika kuheshimu jinsia.
Nimezungumza
“kupiga goti” hapo juu na sio magoti. Kupiga goti kwanza ujulikane ni umoja na
si wingi; hii ikiwa na maana ya kuwa haijalishi ni nani anatakiwa kutekeleza
hicho kitendo kati ya mwanaume au mwanamke, bado inatakiwa tafsiri ijulikane
kwanini unafanya hivyo. Kwanza hutakiwi kupiga magoti yote mawili. Kumbuka
kupiga magoti ni ishara ya kunyeyekea kwa aliyekuzidi nafasi. Kwa lugha
nyingine ni kama kusujudu.
Katika
utamaduni wa Kiyahudi na Kibiblia pia, anayepaswa kusujudiwa ni Mungu peke
yake; lakini hii haina maana kuwa kupiga magoti mbali na mbele ya uso wa Mungu
haitakiwi isipokuwa iwe na tafsiri ya kutosujudia hicho kitu kiasi cha
kuichukua nafasi ya Mungu kwenye maisha yako. Kiyahudi aliyetakiwa kupigiwa
magoti mbali na Mungu ni mtu mwenye cheo kikubwa, mfano mtumwa mbele ya bwana
wake; huyu alipiga magoti na kumbusu bwana wake miguu. Hata hivyo ishara ya
kuheshimu inaoneshwa pia kwa wanaolingana vyeo ambao wao hawakupigiana magoti
isipokuwa walipeana busu mashavuni.
Kitendo
cha kupiga goti kwa mguu mmoja kilionekana kwa watumishi ambao wanafanya kazi
ya Mungu pamoja lakini mmoja akiwa kwenye nafasi ndogo (junior minister) basi
alitakiwa kumsujudia mwenye nafasi kubwa (senior minister) walipokutana na
kusalimiana ili kufanya huduma pamoja. Na hii inaonekana mpaka leo hasa kwa
dhehebu la Roman Catholic na kidogo Lutheran ingawa wao hawapigi goti bali
aliye mdogo husuka kidogo madhabahuni au kusogea mbele kidogo ya kuhani mkuu
hasa wakati wa kutoa Baraka za Utume mwisho wa Ibada.
Sasa
basi, kwa mtindo huu huu wa kuhani mkuu na mdogo kwenye huduma ndio huo huo
unaotakiwa kuchukuliwa kwenye uchumba. Nasema hivi kwa sababu kwenye ukuhani
wote bila kujali ukubwa au udogo kwa Mungu ni Makuhani na wapo sawa isipokuwa
kibinadamu wanaoneshana heshima na si kuabudiana. Kadhalika na kwenye uchumba,
ingawa kuna tofauti kidogo ambayo hiyo tofauti itaegemea kwenye jinsia ipi
ipige goti na hapo ndipo yalipo majibu.
Tunaamini
kwamba mpaka wawili wakutane na kuvisha pete kuna mkono wa Mungu umehusika
ingawa si lazima iwe hivyo japo inatakiwa iwe hivyo. Nazungumza kwa wale ambao
Mungu ameamua kuwakutanisha kama mume na mke mwema. Kama ni hivyo, hawa ni kama
makuhani na katika hao mkubwa na mdogo hapimwi kama kuhani wa madhabahu (ambao
wanapimwa kulingana na elimu ya kuhani au nafasi yake kwenye kanisa bila kujali
jinsia yake). Hawa (wenzi) wanapimwa kwa jinsia kulingana na mpangilio wa
majukumu Kimungu kati yao.
Kwa
mujibu wa Biblia, ni dhahiri na tutakubaliana kwamba Mungu aliwaumba mwanaume
na mwanamke pamoja kwenye mawazo yake, lakini kiuhalisia alianza kumuumba
mwanaume kwanza kisha baadae ndipo alipokuja kumuumba mwanamke kutoka kwenye
ubavu wa mwanaume. Hii tunaipata tunaposoma Kitabu cha Mwanzo sura ya kwanza na
ya pili.
Biblia
pia inaeleza kuwa mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanaume, lakini mwanaume
aliumbwa kwa ajili ya Mungu na kamwe si kwa ajili ya mwanamke (1Kor. 11:9). Na
pia mwanamke alihukumiwa kuwa chini ya mwanaume na kutawaliwa na mwanaume
(Mwanzo 3:16).
NUKUU ZA BIBLIA:
Maana
mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume. Wala
mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya
mwanamume. – 1WAKORINTHO 11:8-9
Akamwambia
mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa
watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. – MWANZO 3:16
Baada
ya kutazama nafasi ya mwanamke na mwanaume hebu tutazame majukumu yao wanapokuwa
pamoja kwa kuunganishwa na upendo. Katika hili mwanaume amepewa jukumu la
kumpenda mwanamke na mwanamke yeye amepewa kumtii mwanaume. Kutii ni
kunyenyekea na kufuata lile ambalo utaagizwa. Sasa si mpaka aelekezwe jambo,
lakini mwanamke anatakiwa kila wakati kuonesha namna anavyomheshimu mwanaume na
mwanaume anatakiwa kufanya kila njia kumwonesha mwanamke kuwa anampenda kwa
vitendo na hata kauli. Kupenda si kunyeyekea, kupenda ni kupenda na sifa za
upendo zipo kwenye 1Wakorintho 13. Hapo naomba tuelewane, hahahahaha (nacheka
kidogo). Hebu turejee Maandiko tena:
Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha
mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Enyi
waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa
ajili yake; - WAEFESO 5:22,23,25
Baada ya hayo tutazame tena ni nani anakuja kwa mwenzake,
ni mwanaume anakwenda kwa mwanamke ama ni mwanamke anakwenda kwa mwanaume? Hapa
niseme wazi kuwa wanakutana (hahahahaha, nacheka tena). Na katika hili si
mawazo yangu bali Biblia inasema, “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba
mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha
babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata
wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu,
mwanadamu asiwatenganishe.” (Mt. 19:4-6)
Hapo kwenye nukuu ya Biblia ni wazi kwamba inasema zaidi
juu ya mwanaume kuanza kuondoka. Inaposema “ataambatana na mkewe” ina
maana kwamba huyu mwanamke lazima awe ametoka kwao pia kwa hiyo wanakutana na
kuwa mwili mmoja. Kwanini nimegusa hili? Ni kwa sababu wapo watu wanaodhani
kwamba wanawake hufuatwa, ni kweli hufuatwa lakini na yeye pia hutoka na
kuitikia wito wa kufuatwa. Na kule kufuatwa tu kwa maana ya mwanaume kuanza
kuonesha kumchagua huyu mwanamke, basi ni heshima kubwa sana huyu mwanamke
anakuwa ametendewa na huyu mwanaume kwa maana mwanamke ni kwa ajili ya mwanaume
na mwanaume kwa ajili ya Mungu hivyo ni kama upendeleo fulani huyu mwanamke
anakuwa ametendewa. Na ndio maana Biblia kwenye Kitabu cha Isaya inaita kitendo
hiki kama kusitiriwa aibu (Isaya 4:1).
Mwanamke asipofuatwa na mwanaume ili kuolewa, Biblia
inatafsiri kwamba huyu mwanamke ni kama yupo kwenye aibu. Hivyo mwanaume
anapomfuata ili kutaka kumwoa basi anakuwa amekuja ili kumsitiri aibu yake. Sasa
unaweza kujiuliza; kati ya msitiri aibu na msitiriwa aibu ni nani yupo juu ya
mwenzake? Hakika ni msitiri ambaye ni mwanaume. Na ndio maana Biblia inasema
kwamba itatokea nyakati wanaume watakuwa wachache, na ikiwa itatokea mwanamke
hajasitiriwa (hajaolewa sasa), itafika wakati wanawake saba watamwendea
mwanaume mmoja na kujigharamia kila kitu ili mradi tu aitwe kwa jina la huyo mwanaume
na kusitirika aibu yake. Kwa maana hiyo mwanaume anakuwa kitu cha thamani sana
kwa mwanamke:
Na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja
wakisema, Tutakula chakula chetu, na kuvaa nguo zetu wenyewe, lakini tuitwe tu
kwa jina lako; utuondolee aibu yetu. – ISAYA 4:1
Ninaposema hizi hoja silengi kumnyanyapaa mwanamke hata
kidogo, hapa tafadhali nieleweke vema kabisa. Najua wanawake ni jeshi na
mashujaa sana tena wenye uwezo mkubwa na ndio maana wakawekwa kama wasaidizi,
maana hakuna msaidizi ambaye ni dhaifu, lazima awe na nguvu na uwezo kuliko
anayesaidiwa. Tena wanawake wamewekwa pia makusudi ili kuwalinda wanaume.
Biblia inasea kwenye Yeremia 31:22b kuwa, “Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya
duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.” Tena hawa wanawake ndio watu wa kwanza kueneza
Habari Njema ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, hivyo si viumbe vya mchezo
mchezo. Lakini pamoja na hayo, tunaangalia nafasi kati ya mwanaume na mwanamke
wanapokuwa pamoja, Mungu ameweka utaratibu gani? Hapo ndipo tunaona Mungu
amempa mwanaume majukumu mengi zaidi kuliko mwanamke na hii inatoa pia fursa ya
mwanaume kuwa juu ya mwanamke lakini kwa kumpenda, kumthamini na kumchukulia
kama chombo dhaifu. Biblia inaongeza hivi, “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu
kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi
pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.” – 1PETRO
3:7
Kwa hoja hizo hapo juu, ni wazi sasa umepata jibu kwamba ni
nani anapaswa kupiga goti wakati wa kuvisha pete ya uchumba. Kama bado
nikuambie kuwa ni MWANAMKE NDIYE ANAYEPASWA KUPIGA GOTI WAKATI WA PETE YA
UCHUMBA kwani kwa kufanya hivyo atakuwa anaonesha utii na heshima kwa mwanaume ili
kutimiza jukumu lake la kwenye Biblia.
Asante, naitwa Mw. Benson Mmari
Ikiwa kuna maswali zaidi, wasiliana name kwa WhatsApp na.
+255 652 262 137
Chapisha Maoni
Enenda kwa hekima, ukijua ni yapi yaliyo mapenzi ya Mungu huku ukiukomboa wakati. Install Bewisa App kwenye PlayStore kwa maarifa zaidi.
- EV. BENSON W. MMARI, +255 768 111 279